Sawa, tuendelee kidogo… “Robot, Polyamory na Chura”

14 05 2009

Niliamua kuitika mwito wa Bomseh na kuwafunulia kidogo maisha ya Serina. Nawashukuru kwa maoni yenu na nim’amua kuendeleza kidogo tu!

Kwa kunitembelea hapa nawaona kama ndugu zangu na pia naamini duniani hakuna siri, ingawa sote twapenda kujistiri kwa kuyafunga midomo yetu.

Wachache wenu m’meandika kuhusu hotuba zinazotolewa kwenye matanga, yangu sitaki iwe mistari inayosimua historia yangu… kaenda shule sijui wapi, alipenda ushairi, amewaacha wanaume kadhaa na watoto kadhaa…. la hasha, sitaki. Sitaki hotuba ya aina yoyote… Maisha yangu na kazi zangu nataka zijizungumuzie.

Nimefurahia kujua kuwa kati yenu kuna wanaume wasioogopa kuingia jikoni na pia kusaidia katika shughuli nyumbani. Kama mwanamke, binti, mama, dada … nawashukuru kwa hilo maana wanawake tumezoea kuvumilia mengi maana hatutaki kuonekana wavivu. Na ninaomba tafadhali muwasaidie wenzenu na shughuli nyumbani hata kama mnawalipa, kazi ya nyumba huwa haiishi na hata akina yaya, boi, ‘robot’ na waajiriwa wengine wote ni binadamu, na huchoka. Uliza mwafrika aliyeishi ughaibuni na hana starehe za wafanyikazi nyumbani…

Tuendelee na swala la “Polyamory” … sijui tafsiri yake kwa kiswahili ni ipi … waswahili mpo?

Huwa na keti na kuwaza sana kuhusu mila na desturi zinazopatikana kotekote duniani. Hili wazo la ‘Polyamory’ lilijitokeza baada ya kutazama filamu moja ya kimaasai, shughuli za kuchoma mkuki mlangoni, na pia kwa kusikia visa vya kina mama na mazubeda maishani mwao… mwamkumbuka Zubeda?

Sidhani kuna chochote kibaya na uhusiano wa wazi kati ya watu wazima ilmradi wajikinge kutokana na magonjwa ya zinaa na pia waweke wivu kuleeee mpakani kule. Mwenzangu kwa mfano akitaka kuwa na mke wa pili, bora awe na sababu halisi, siwezi mkataza… amini usiamini! Naamini ya kuwa ” there is always enough love to go around ” … au? Labda nilisheruka kichwa na sijajitambua :D

Kaka Bwaya naye aliulizia ‘profile ya a good frog‘ . Kwanza neno frog nililitumia sio kutokana na umbo la chura bali nilikumbuka hadithi ya ‘The princess and the frog’ na pia filamu ya Shrek. Huwa natazama sana filamu za watoto (mazoea).

Kabla sijaandika kuhusu chura wangu, ningependa kuwakumbusha ya kuwa Penzi halilazimishwi ni mtu kwa mtu wake au Marazz alivyojibu, kila jini na mbuyu wake.

Mwenzangu tumefahamiana mda mrefu. Tulikutana hukuhuku nilipo sasa lakini njia zetu zikaenda panda. Alirudi nyumbani Afrika nami nilibaki huku. Hatukujua kuwa pepo zingeturusha pamoja tena.

Ni mtu mwenye upendo sana na mvumilivu kupita kiasi. Mcheshi. Hanioni tu kama mwenzake lakini pia kama mtu binafsi. Kama Serina.

Kuna vitu vingi ninavyoona anapozungumuza na watu wa kila aina, mimi, marafiki na hata familia. Ana heshima. Mkarimu. Mungwana kweli… Hana kiburi… ningependa kuendelea lakini machozi yananilenga machoni…

Weekendi njema!


Actions

Information

11 responses

15 05 2009
ringojr

Serina huku mtandao unasuasua.

15 05 2009
Serina

Pole.

15 05 2009
Chib

Nimeipenda blog yako.
Kwenye ushirikiano ongeza na Uganda hata Kama Mu-7 amewanyang’anya maji yanayozunguka Migingo.

Kigali, Rwanda

15 05 2009
Bwaya

Hongera sana Serina kujaaliwa mwandani akufaaye. Mie huamini kabisa kuwa mapenzi yana nafasi kubwa katika mchakato wa maisha yetu. Furaha inayoanzia katika familia, husambaa na kutufuata madarasani, maofisini, mashambani na kwingineko. Kule kuamini kuwa ‘chura uliyenaye’ anakufaa, kunaanisha utimilifu wa furaha hiyo.

…mambo haya ya kibinafsi huwa hayapati nafasi ya mbele kwenye blogu zetu. Japo nayo ni ya muhimu sana. Kwa hivyo ilikuwa bahati sana kusikia mawili matatu kukuhusu wewe kama Serina. Nimejifunza mengi mazuri kupitia simulizi lako binafsi na bila shaka nitaendelea kusikia zaidi na kujifunza zaidi.

Kingine. Nimefurahia sana mtazamo wako kuhusu pesa. Kwa mukhtadha wa kiafrika, pesa ni za jamii. Ukizipata, maana yake jamii nayo imepata. Pesa ziwasaidie na wanaotuzunguka. Laiti ingekuwa hivyo kwa wengi wetu, hizi mbizi za ufisadi zingekuwa na maana nyingine tusiyoifahamu.

Hilo ni la msingi.

18 05 2009
Serina

@ Chib: Asante na Karibu.

@ Bwaya: Asante.
Kweli unavyosema, wengi hatupendi kuweka mambo ya kibinafsi wazi lakini watu mkishezoeana inakuwa rahisi kidogo. Kisha swala la pesa na kutunzana kijamii siku hizi sijui imekuwa vipi na ninakubaliana na uliyoyasema hapo juu.

19 05 2009
kaasa

Hongera Serina. :-)

22 05 2009
Fadhy Mtanga

Serina nini jamani?
Lazima u furahani,
Huyo wako mwandani,
Yu muhimu duniani.

Mapenzi raha rahaye,
Umpate ye akufaaye,
Raha kamili akupaye,
Furaha moyoni akupaye.

27 05 2009
LUIHAMU

Habari Serina,

Kimya kimezidi
ingawa majukumu nayo yamezidi
jitahidi urudi.

1 06 2009
yasinta

Hongera sana Serina
kwa kumpata akufaaye
jag är gla för din skull

1 06 2009
ringojr

kimya kingi kina kishindo kikubwa.

15 06 2009
Ria

A frog by any other name is still a frog I guess? Lol, just messing with your brains :D

Leave a comment