Rafiki…
narudia neno hili
polepole
nikionja utamu wake
n’natabasamu peke yangu
kwani najua kuwa
rafiki huyu…
ni rafiki wa kweli
milango mingi tum’pitia
madirisha vilevile
um’nisaidia kukusanya kamba zangu
na kuzifuma pamoja
mkeka um’pendeza
bila we rafiki
sijui ungefanana aje.
Rafiki…
n’natabasamu kwani
husiti
kuniambia ukweli ulivyo
yawe machungu
au
yawe matamu
na cha muhimu kabisa
wanipa sikio lako
iwe kwa dakika chache
au masaa kabambe
Rafiki…
washangilia nami
mazuri yanapotokea
na kuniliwaza
n’napopatwa na mazito
Rafiki…
nakupenda.

