Demokrasia

28 06 2007

uchaguzi kidemokrasia…

yu wepi tuliyemchagua’si?

 

demokrasia yapeleka nchi mbele…

mafunzo ya wakoloni tushazoea,

bila demokrasia msaada ham’tapokea,

wafuateni wajuao njia msijepotea!

mwasema tuithamini demokrasia…

madawa hospitalini twasubiri,

msingi kwa vijana mliahidi,

barabara vijijini zafika lini?

endesha pajero demokrasia…

petroli gari wajaziwa,

nyumba kodi walipiwa,

masikini naye an’angalia!

lala hotelini demokrasia…

chokora si tatizo langu ’sha kwambia,

kazi yako si ulijichagulia?

niambie kingine kisicho gasia.

umoja ni nguvu twajivunia…

kura zenu mlinipa uhakika gani?

sie nyie mwajiita wapinzani?

mbona mwanililia’mi? Jameni!

majimbo kidemokrasia…

msiukaribie mpaka wetu!

msijichanganye na wakwetu!

msinitatize na shida zenu!!

kama demokrasia wapishe walioteuliwa….

wanichochea bahati haikuwa yako,

uchaguzi ujao labda zamu yako,

si demokrasia kwa wote?





Buriani

25 06 2007

Wakati umewadia

machozi hayatasaidia

moto umefifia

sikutaka kuuzima

mtindo wa maisha

buriani lazima





Sitarudia tena

15 06 2007

Wiki mwisho ukiwadia…

Sitaki riziki hata kufikiria!

Kazi mazoea kila jumaa kuisingizia,

kosa lile sitaki tena kulirudia.

Hadithi lile si la kukusimulia…

lakini wataka kujua mbona nalia.

Nyumbani upweke ul’kuwa mtindo nakwambia…

mtindo huo kuuvunja wiki mwisho ulikuwa.

Jumamosi usiku lazima nje nilitembea,

kuna binti moja mrembo niliyemchochea…

Jumapili asubuhi sikumbuki lilotokea,

hata jina la kwanza akilini ‘linipotea.

N’lipomtazama mjusi yule akijipodoa…

mawazo chungu tele, ni lini nil’potea?

Usingizi ul’nitoroka sebuleni al’potokea,

malipo ‘kaitisha haki yake ‘kaniambia!

N’na wasiwasi mdudu labda nim’uokota…

ulevi wangu mpira mbona sikuutumia?

Nyumbani upweke mtindo tena umekuwa…

Mwisho wa wiki sitaki tena kuutambua!





Wanifanyani?

13 06 2007

Uvumilivu wako…

wanifanya’mi mvumilivu,

Utu wako…

wanionyesha nia yako,

Ustaarabu wako…

wanipa joto,

Nguvu un’yoonyesha…

wanipa misisimiko,

Ucheshi wako…

wanipa raha,

Usamehevu wako…

wanipa amani,

Subira ulilo nalo…

wan’tuliza moyo.

Nakupenda lakini…

Umbali wako,

wan’chosha.





Raha ya pesa

9 06 2007

Mwisho mwezi keshafika,

wafanyi kazi wameridhishwa,

centi mikononi tele…

leo bibi hatapiga kelele.

‘Madamu’ tafadhali chukua taxi…

garama kwangu us’jali!

Majamaa njooni tupige raundi…

vilabu, bia na chagudoa, tuanzie wapi?

Raha ya leo mbona fupi imekuwa?

Ni matatizo tele si wajua…

Kimbia hapa, kimbia pale,

nunua hiki, nunua kile…

Watoto mavazi wan’hitaji,

karo shuleni si utani,

umeme ut’katwa usipowahi,

Bibi naye we! ni mkali!

Mashemeji nao mlangoni,

wezi nao ukingoni…

Sitoo chakula hata sijajaza!

Pesa nikiwa nawe sina raha!

Mboga chemsha na sima kiresheni,

‘bucha’ sipitii ila nifikishwe’mi kichinjoni…

Viatu bila rangi wiki mbili zishapita,

Gari nalo benki wenye mnada walishewaita.

Boi na yaya virago wash’funga,

Bibi kaniacha an’sema mie mjinga!

Mpangishaji naye kampu mlangoni keshapiga,

Pesa bila wewe sina raha!





Niite utakacho

5 06 2007

Niite binti fulani…

kwa maana uhusiano kati

ya wazazi wangu,

ndio kilichonileta duniani.

Niite mama…

kwa maana umeona,

sifa hiyo inanitosha…

ulezi wa wana

nd’o kazi ya kwanza.

Niite mwana…

kwa maana umri wako,

na busara ulionayo,

na kwa heshima kwako…

nitaaitika.

Niite mwanamke…

kwa maana una nia

ya kukiri kuwa

mimi sio mme.

Niite kipepeo cheusi,

kwa maana najisifia

uhuru wangu,

na rangi yangu…

sitotupilia mbali historia yangu.

niite dada,

niite ndugu,

niite mpendwa,

niite mpenzi…

niite adui,

niite kafiri,

niite jasiri…

niite mzembe,

Niite utakacho…

kwa sababu unazozijua mwenyewe…

hautanibadili nilicho.